Maandalizi BBA3 murwaaa
Lile shindano linakoseshaga wengi usingizi kutokana na msisimko wake la 'Big Brother Africa' linakaribia kuanza tena kwa mwaka huu, imefahamika.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya MultiChoice tawi la Tanzania, Lucy Kihwele alitoa wito kwa wale wote ambao walijiandikisha kushiriki kwenye shindano hilo kuwasilisha maelezo yao kwenye ofisi yake jijini Dar es Salaam.
Kihwele alisema washiriki hao walitakiwa kuwakilisha fomu zao mwishoni mwa mwezi Aprili.
“Kwa mujibu wa Mkurugenzi ambaye anashughulikia nchi zilizoko Ukanda wa Jangwa la Sahara barani Afrika, Joseph Hundah, alisema kwamba kutokana na kusuasua kwa kurejeshwa maombi hayo watalazimika kuongeza muda,” alisema Kihwele.
Aliongeza kwa kusema kuwa huu ni msimu wa tatu wa shindano hilo hivyo kutokana na umaarufu liliojizolea wamepata maombi mengi kutoka nchi shiriki ambayo yote yatafanyiwa kazi.
Pamoja na kuwa maombi ni mengi, lakini washiriki wanaotakiwa ni 12 tu watakaoingia kwenye jumba la BBA3 2008, huku Tanzania ikiwa na nafasi ya mshiriki mmoja pekee.
Sifa za kushiriki ni kwa yeyote mwenye umri kuanzia miaka 21 na mwenye kuongea kwa ufasaha lugha ya Kiingereza, raia wa nchi husika na mwenye pasi ya kusafiria.
Washiriki wa shindano hili wanatoka kwenye nchi 12 ambazo ni Angola, Botswana, Ghana, Malawi, Namibia, Nigeria, Kenya, Afrika Kusini, Uganda, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
BBA3 inatarajiwa kuzinduliwa Agosti 24 siku ya Jumapili Agosti 24 ambapo washiriki watakaa kwa muda wa siku 91 katika jumba maalum nchini Afrika Kusini na kuhitimishwa Novemba 23 mwaka huu.

Gonga hapa kutoa
maoni yako kuhusu story hii...!!!

Gonga hapa kusoma
maoni hayo...!!!
Mtumie Rafiki |
Print nakala